Jan 19, 2024 07:38 UTC
  • Kikao cha leo cha wakuu wa NAM Uganda; Iran yataka jumuiya hiyo itilie mkazo kuihami Palestina

Mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM unafanyika leo katika mji mkuu wa Uganda, Kamapala huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwataka wanachama wa jumuiya hiyo kutilia mkazo uungaji mkono wao kwa taifa linalodhulumiwa la Palestina.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Mohammad Mokheber ndiye anayemwakilisha Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu katika mkutano huo wa NAM ambao leo unashuhudia Uganda kuwa mwenyekiti wa mzunguko wa jumuiya hiyo.

Marais wa nchi waliowasili Kampala kwa ajili ya mkutano huo ni pamoja na William Ruto wa Kenya, Salva Kiir Mayardit wa Sudan Kusini, Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia, Ismail Omar Guelleh wa Djibouti, Emerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Eodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea, Ranil Wickremesinghe wa Sri Lanka, Roch Wamytan wa New Caledonia na Zeljka Cvijanovic wa Bosnia Herzegovina. 

Reza Najafi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya Sheria na Kimataifa.

 

Nchi nyingine zimewakilishwa na Makamu wa Marais na kwa upande wa nchi kama Tanzania, Rwanda, Algeria, Nepal, The Bahamas na Mali, zimewakilishwa na Mawaziri Wakuu. Tayari viongozi wote hao wako mjini Kampala hivi sasa kwa ajili ya mkutano huo.

Kwa upande wake Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewataka wanachama wa NAM kutilia mkazo mshikamano wao na taifa linalodhulumiwa la Palestina, huku mashambulizi ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Ghaza yakiendelea kupoteza maisha ya Wapalestina wasio na hatia katika eneo hilo la pwani lililozingirwa kila upande na Israel.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya Sheria na Kimataifa, Reza Najafi, aliyasema hayo Jumatano akihutubia katika Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Juumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) mjini Kampala, Uganda.

Katika sehemu moja ya hotuba yake, Najafi alisema: "Ujumbe wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa lazima uwe mkali na wa wazi ili kuonyesha kwamba jumuiya hiyo inasimama pamoja na taifa la Palestina."

Tags