Afrika Kusini: Mwanamume akiri kuwasha moto ulioua watu 76
Mwanamume mmoja amekamatwa nchini Afrika Kusini na atakabiliwa na makosa 76 ya mauaji baada ya kuuambia uchunguzi kwamba alianzisha moto mbaya ulioteketeza jengo huko Johannesburg mwaka uliomalizika majuzi.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 29 amekiri kwamba aliwasha moto huo wakati akijaribu kuutoa mwili wa mtu ambaye alikuwa amemnyonga katika jumba la ghorofa kwa amri ya mlanguzi wa dawa za kulevya.
Ungamo hilo la kushangaza linafuatia uchunguzi wa umma kuhusu moto huo ulioteketeza Jengo la Usindiso huko Marshalltown ambao ulisababisha vifo vya watu 76, huku mwanamume huyo ambaye jina lake halikutajwa akisema alimwaga petroli kwenye mwili wa mwathiriwa wake na kuuchoma.
Uchunguzi huo unataka kubaini ni nini kilisababisha moto huo na ni dosari gani za usalama zinaweza kusababisha watu wengi kufariki dunia.
Mwanamume huyo ambaye alikuwa mkazi wa jengo hilo, pia anakabiliwa na mashtaka ya makosa 120 ya kujaribu kuua na shtaka la kuchoma moto.
Moto huo uliosambaa katika jengo hilo ni moja ya majanga makubwa zaidi nchini Afrika Kusini, na ulivutia mazingatio ya dunia kwa tatizo la kile kinachoitwa majengo yaliyotekwa nyara mjini Johannesburg, ambayo yametelekezwa na mamlaka na kuchukuliwa na wamiliki wa nyumba kinyume cha sheria.
Tukio hilo pia lilizua hasira za umma nchini Afrika Kusini kutokana na serikali kuonekana kutokuwa na uwezo wa kukomesha uvamizi haramu wa majengo hayo.