ZANU-PF: Mugabe hatojiuzulu licha ya maandamano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10792-zanu_pf_mugabe_hatojiuzulu_licha_ya_maandamano
Chama tawala nchini Zimbabwe cha ZANU-PF kimesema Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo hatajiuzulu licha ya mgomo wa wafanyakazi na maandamano ya wananchi kulalamikia uongozi wake na hali mbaya ya uchumi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2016 00:18 UTC
  • ZANU-PF: Mugabe hatojiuzulu licha ya maandamano

Chama tawala nchini Zimbabwe cha ZANU-PF kimesema Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo hatajiuzulu licha ya mgomo wa wafanyakazi na maandamano ya wananchi kulalamikia uongozi wake na hali mbaya ya uchumi.

Ignatius Chombo, Katibu wa masuala ya Utawala wa chama hicho amesema serikali ya Rais Mugabe haitikiswi na wimbi hilo la maandamano na kelele za wanaharakati na wapinzani.

Chombo amesema na hapa tunamnukuu: "Tunajua kwamba maandamano yanayofanyika haswa mjini Harare yanaungwa mkono kikamilifu na madola ya Magharibi licha ya mashirika ya kijamii yanayohusika kujipachika majina ya kuonyesha kuwa ni wafanyakazi na wachuuzi wa nchi hii." Amesema njama za nchi za Magharibi za kujaribu kumpindua madarakani Rais Mugabe zitagonga mwamba na kwamba mashinikizo hayo hayawezi kuifanya ZANU-PF ibadili misimamo yake. Dumisani Nkomo, msemaji wa harakati ya Crisis in Zimbabwe Coalition amesema mgomo wa wafanyakazi na maandamano hayo yanadhihirisha machungu ya wananchi na namna walivyochoshwa na utawala wa Mugabe.

Wapinzani wanamtuhumu Mugabe mwenye umri wa miaka 92, kuwa anaendesha nchi kiimla mbali na kushindwa kutatua matatizo ya kiuchumi na ukosefu mkubwa wa ajira.

Mugabe ameitawala Zimbabwe tangu ilipojinyakulia uhuru mwaka 1980 na tayari chama tawala cha ZANU-PF kimemteua awanie tena urais mwaka 2018.