Misri yatishia kusimamisha Mkataba wa Camp David endapo Israel itashambulia Rafah
Feb 12, 2024 10:19 UTC
Misri imetishia kusitisha mkataba wa amani wa Camp David iliosaini na utawala wa Kizayuni wa Israel iwapo wanajeshi wa utawala huo ghasibu watapelekwa katika mji wa mpakani wa Gaza uliofurika watu wa Rafah na kusema mapigano huko yanaweza kulazimisha kufungwa kwa njia kuu ya kusambazia misaada katika eneo hilo.
Tamko la kutishia kusimamisha makubaliano hayo, lilitolewa jana Jumapili na maafisa wawili wa Misri baada ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu kudai kuwa kutuma wanajeshi huko Rafah ni muhimu ili "kushinda" vita vilivyodumu kwa miezi minne sasa dhidi ya harakati ya muqawama wa Palestina Hamas.
Zaidi ya nusu ya wakazi milioni mbili na laki tatu wa Gaza wamekimbilia Rafah kuepuka hujuma na mashambulio ya kinyama ya Israel katika maeneo mengine, na wamefurika kwenye kambi kubwa za mahema na makazi yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa karibu na mpaka.
Misri inahofia kumiminika kwa wingi ndani ya ardhi yake mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Kipalestina ambao huenda wasiruhusiwe kurejea tena makwao.
Uvamizi wa ardhini huko Rafah unaweza kukata mojawapo ya njia pekee za kusambaza chakula na vifaa vya matibabu vinavyohitajika sana katika eneo la Gaza.
Umoja wa Mataifa umesema Rafah, ambayo kwa kawaida ni makazi ya watu wasiofika laki tatu, hivi sasa imeshapokea Wapalestina milioni moja na laki nne waliokimbia mashambulio ya utawala wa Kizayuni; na kwa mujibu wa UN eneo hilo "limefurika watu kupita kiasi".
Mkuu wa Sera za Nje za Umoja wa Ulaya Josep Borrell ameandika kwenye mtandao wa X kuwa: "mashambulio ya Israel dhidi ya Rafah yatasababisha janga la kibinadamu lisiloelezeka na mvutano mkubwa na Misri".
Utawala wa Kizayuni wa Israel na Misri zilikuwa zilishawahi kupigana vita vitano kabla ya kutia saini Mkataba wa Camp David mwaka 1978 kwa usimamizi wa rais wa wakati huo wa Marekani Jimmy Carter. Mkataba huo unajumuisha vifungu kadhaa vinavyosimamia uwekaji wa vikosi katika pande mbili za mpaka.
Viongozi wa Misri wanahofia kwamba ikiwa makubaliano ya mpaka yatavunjwa, wanajeshi wake hawataweza kuzuia wimbi la Wapalestina watakaolazimishwa kuhama Rafah na kumiminika kwenye Jangwa la Sinai.../
Tags