Feb 16, 2024 02:46 UTC
  • Odinga asema yuko tayari kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU

Kinara wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga ametangaza rasmi azma yake ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).

Katika kikao na waandishi wa habari mjini Nairobi jana Alkhamisi, Odinga alisema yuko tayari kushikilia cheo hicho, kwa kutulia maanani uzoefu alioupata akiwa Mwakilishi Mkuu wa AU katika masuala ya miundombinu.

Odinga ambaye alikuwa ameandamana na rais wa zamani wa Nigeria, Olesegun Obasanjo kwenye mazungumzo hayo na waandishi wa habari amesema amefanya mashauriano ya kina na wadau mbali mbali kabla ya kufikia uamuzi huo.

Odinga ambaye amegombea mara kadhaa kiti cha urais nchini Kenya bila mafanikio amesema, "Kuhudumu kama Mwakilishi Mkuu wa Miundombinu wa Umoja wa Afrika kulinipa fursa ya kujifunza mengi kuhusu kila taifa la Afrika. Naamini kwa kushirikiana, tunaweza kuikomboa Afrika."

Mwenyekiti wa Tume Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat 

Kinara huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini Kenya ODM alihudumu katika wadhifa huo baina ya mwaka 2018 na Februari mwaka jana, wakati ambapo muhula wake wa kuhudumu ulimaliza ghafla na katika mazingira ya kutatanisha.

Obasanjo huku akiunga mkono azma hiyo ya Odinga ya kuwania kiti hicho amesema, wakati umefika kwa cheo hicho kutwaliwa na kiongozi mwenye tajriba kutoka mashariki mwa bara Afrika.

Muda wa kuhudumu Mwenyekiti wa sasa wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat ambaye amekuwa kwenye cheo hicho kwa mihula miwili tokea mwaka 2017, unamalizika mwaka huu. 

 

 

Tags