Feb 20, 2024 07:06 UTC
  • Ghannouchi, kiongozi wa upinzani Tunisia aliyefungwa jela aanza mgomo wa kususia kula

Rached Ghannouchi, mwanasiasa mashuhuri wa upinzani nchini Tunisia na kiongozi wa chama cha Ennahda, ameanza mgomo wa kususia kula akiwa kifungoni jela kuonyesha mshikamano na wanaharakati wenzake wanaopinga serikali.

Kwa mujibu wa timu ya mawakili wanaowakilisha upinzani, hatua hiyo imechukuliwa kama njia ya kupinga kuendelea kuzuiliwa kwa viongozi wa upinzani.

Ghannouchi, mwenye umri wa miaka 82, kwa muda mrefu amekuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Kais Saied na utawala wake. Mwaka jana, alikamatwa kwa tuhuma za uchochezi dhidi ya polisi na madai ya kuhusika katika njama dhidi ya usalama wa serikali.

Katika taarifa iliyotolewa na timu yake ya wanasheria, Ghannouchi amewataka wananchi wa Tunisia kuzingatia kanuni za kidemokrasia, akisisitiza umuhimu wa uhuru wa watu binafsi na kuwa huru mhimili wa Mahakama. Licha ya mgomo wake wa kususia kula, Spika huyo wa bunge la Tunisia lililovunjwa na rais Saied amesisitiza kuwa ataendelea kujitolea kutetea Tunisia yenye demokrasia ambayo inajumuisha raia wake wote.

Rais Kais Saied

Upinzani umelaani vikali hatua ya Rais Saied, hasa uamuzi wake wa kulivunja bunge lililochaguliwa mwaka 2021, uamuzi ambao wanauchukulia kuwa ni sawa na kufanya mapinduzi ya kijeshi. Lakini kwa upande wake, kiongozi huyo anatetea hatua zake akiziita kuwa ni uamuzi muhimu wa kurejesha utulivu nchini Tunisia baada ya miaka mingi ya machafuko ya kisiasa.

Wiki iliyopita, viongozi wengine sita wa upinzani walianzisha mgomo wa kususia kula kwa muda usiojulikana ili kushinikiza waachiliwe kwa kuwekwa kizuizini bila ya kufikishwa mahakamani. Pia wametaka kukomeshwa unyanyasaji unaofanywa na vyombo vya mahakama dhidi ya wanaharakati wa kisiasa, waandishi wa habari, na wanachama wa asasi za kiraia.

Viongozi waliowekwa kizuizini, akiwemo Jawher Ben Mbarak, Khayam Turki, Ghazi Chaouachi, Issam Chabbi, Abdelhamid Jalasi, na Rida Belhaj, walikamatwa kwa tuhuma za kupanga njama dhidi ya usalama wa serikali.

Upinzani unamshutumu Rais Saied kwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na kudhoofisha taasisi za kidemokrasia kupitia mageuzi yake ya kikatiba. Saied, hata hivyo, anashikilia kuwa hatua zake ni muhimu kuilinda Tunisia na kuvurugika kwa utulivu.../

 

Tags