Feb 25, 2024 09:56 UTC
  • Sudan yapuuzilia mbali madai ya Marekani dhidi yake

Serikali ya Sudan imekosoa vikali taarifa ya Marekani inayotuhumu serikali ya Khartoum kwamba inazuia watu nchi humo kufikishiwa misaada ya kibinadamu.

Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesema, tuhuma za Marekani dhidi ya Jeshi la Taifa la Sudan SAF na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF ni za urongo na hazina msingi wowote.

Taarifa hiyo imetupilia mbali madai hayo ya Marekani dhidi yake na kusisitiza kuwa, serikali ya Khartoum imeazimia kufungamana na Tangazo la Jeddah la Kuwalinda Raia lililosainiwa mnamo Mei 11 mwaka uliopita 2023.

Serikali ya Sudan imesema haielewi ni kwa nini taarifa hiyo ya Marekani imekwepa kulaani moja kwa moja na kwa uwazi uhalifu na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imeeleza bayana kuwa, tuhuma hizo za Marekani kuhusu kuzuiwa misaada ya kibinadamu kuwafikia Wasudan wanaostahiki hazina msingi wowote.

Mapigano nchini Sudan

Siku ya Alkhamisi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa taarifa ikidai kuwa, Jeshi la Taifa la Sudan SAF na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vinazuia wahusika kufikiwa na misaada ya kibinadamu katika hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Haya yanajiri huku vita vya kuwania madaraka vikiendelea kuchachamaa nchini Sudan. Juhudi za kieneo na kimataifa za kuzishawishi pande mbili hasimu kuketi kwenye meza ya mazungumzo na kutatua tofauti zao hazijafua dafu mpaka sasa.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), watu zaidi ya 13,000 wameuawa tangu mapigano baina ya pande hizo mbali yaanze nchini Sudan katikati ya Aprili mwaka uliopita 2023.

Tags