Rwanda 'kuwatimua' wakimbizi wa Burundi
Rwanda imesema itaanza kukabidhi wakimbizi raia wa Burundi walioko nchini humo kwa nchi ambazo ziko tayari kuwapokea.
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na Ofisi ya Msemaji wa Serikali imesema kuwa, tayari serikali ya Kigali imeanza kufanya mazungumzo na washirika na jamii ya kimataifa kwa ujumla kuhusu namna ya kukabidhi wakimbizi wa Kirundi wapatao 75,000, kwa njia mwafaka na bila kuhatarisha usalama wao kwa nchi ambazo ziko tayari kuwapokea. Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Msemaji wa serikali ya Rwanda Loise Mushikiwabo amesema serikali ya Kigali imeshindwa kuhimili gharama za kuwadhaminia usalama na kuwatunza wakimbizi hao na kwamba uwepo wao nje ya nchi yao kunazidi kulemaza juhudi za kuutafutia ufumbuzi mgogoro unaoikumba nchi yao. Hii ni katika hali ambayo, hivi majuzi Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda alikanusha madai yaliyotolewa kwenye ripoti ya Umoja wa Mataifa kwamba nchi yake inatoa mafunzo ya kijeshi kwa wakimbizi wa Burundi ili waweze kuipindua serikali ya Rais Pierre Nkurunziza. Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda amesema Rwanda imekuwa ikiwapokea wakimbizi wa Burundi katika kalibu ya kutekeleza majukumu yake ya kimataifa na ujirani mwema na kwamba inasikitisha kuona Umoja wa Mataifa ukikosa kutambua juhudi hizo na badala yake kutoa madai ya uongo dhidi ya Kigali.