Visa zaidi vya utekaji nyara vyahofiwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i109390-visa_zaidi_vya_utekaji_nyara_vyahofiwa_nigeria
Serikali ya Shirikisho ya Nigeria imeorodhesha shule kadhaa katika majimbo 14 nchini humo kuwa ni maeneo yaliyoko hatarini kushambuliwa na majambazi na wahalifu wenye silaha.
(last modified 2024-03-12T02:15:54+00:00 )
Mar 12, 2024 02:15 UTC
  • Visa zaidi vya utekaji nyara vyahofiwa Nigeria

Serikali ya Shirikisho ya Nigeria imeorodhesha shule kadhaa katika majimbo 14 nchini humo kuwa ni maeneo yaliyoko hatarini kushambuliwa na majambazi na wahalifu wenye silaha.

Hata hivyo Hajia Halima Ilya, Mratibu wa Taifa wa mradi wa shule salama unaoendeshwa na serikali ya Nigeria hakuyataja majimbo hayo 14 yaliyoripotiwa kuwa hatarini kushambuliwa na majambazi na wahalifu wanaobeba silaha. Hajia Halima ameeleza kuwa, taasisi hiyo imekusanya taarifa ambazo zitawasaidia kuchukua hatua za kukabiliana na magenge ya utekaji nyara. 

Tarehe 7 mwezi huu wa Machi majambazi waliokuwa na silaha waliwateka nyara wanafunzi 287 katika mji wa Kuriga jimboni Kaduna, kaskazini mwa Nigeria. Siku mbili baadaye pia majambazi  waliokuwa na silaha walivamia shule ya bweni katika kijiji cha Gidan Bakuso katika Jimbo la Sokoto na kuwateka nyara watoto 15.

Hofu yatanda kufuatia visa vya utekaji nyara Nigeria 

Rais Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria  tarehe 8 mwezi huu alisema kuwa ameyaagiza mashirika ya usalama na ujasusi kuwaokoa waathirika na kuhakikisha kuwa wahusika na vitendo hivyo vya uhalifu wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Idadi ya wanafunzi waliotekwa nyara Nigeria imepindukia zaidi ya 1,400 tangu kundi la wanamgambo wa Boko Haram liwateke nyara wanafunzi 276 karibu miaka kumi iliyopita.