Nchi za Kiafrika zatakiwa zibakie katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC
Asasi mbalimbali zisizo za kiserikali zimetoa wito kwa nchi za Kiafrika kubakia kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa shabaha ya kuunga mkono haki za binadamu barani humo.
Taarifa ya jumuiya hizo imesema kuwa, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ya The Hague Uholanzi ni tumaini la Waafrika na njia pekee ya kuwapandisha kizimbani viongozi mbalimbali wa ngazi za juu barani Afrika waliotenda jinai tofauti ili wakajibu mashtaka.
Wakati huo huo vikao vya utangulizi kwa ajili ya duru ya 27 ya mkutano wa Umoja wa Afrika vinaanza leo katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
Kilele cha mkutano huo kinatarajiwa kufanyika tarehe 16 hadi 18 mwezi huu mjini Kigali.
Miongoni mwa ajenda za vikao vya utangulizi vya mkutano wa 27 wa Umoja wa Afrika ni uwezekano wa nchi za Kiafrika kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi.
Viongozi wa Kiafrika wamekuwa wakiikosoa vikali mahakama hiyo wakisema kwamba, inatumiwa kisiasa na madola ya kibeberu kwani wanaoandamwa zaidi na mahakama hiyo ni viongozi wa Kiafrika.