Mar 20, 2024 11:33 UTC
  • Maafisa wa uchunguzi Afrika Kusini wapekua nyumba ya Spika anayetuhumiwa kupokea hongo

Maafisa wa Kitengo Maalumu cha Uchunguzi nchini Afrika Kusini wamepekua nyumba ya Spika wa Bunge kwa zaidi ya saa tano na kuchukua ushahidi kama sehemu ya uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili kiongozi huyo za kupokea hongo alipokuwa waziri wa ulinzi.

Kufanyika kwa operesheni hiyo ya msako na unasaji katika nyumba Bi Nosiviwe Mapisa-Nqakula, ambaye ni mbunge mkongwe katika chama tawala cha African National Congress, kumethibitishwa katika taarifa kutoka Bungeni.
 
Hata hivyo taarifa hiyo ya Bunge imesema, Mapisa-Nqakula amekanusha kufanya kosa lolote na "kusisitiza kuwa hana la kuficha". Aidha imesema, spika huyo ametoa ushirikiano kwa wachunguzi hao waliofanya upekuzi huo jana Jumanne nyumbani kwake mjini Johannesburg.
 
Taarifa za kufanyika uchunguzi dhidi ya Mapisa-Nqakula mwenye umri wa miaka 67, ziliwekwa hadharani mwezi huu na gazeti moja, ambalo lilisema alishukiwa kupokea dola zisizopungua120,000 kwa njia ya rushwa kutoka kwa mkandarasi wa masuala ya ulinzi kati ya 2016 na 2019.
Jacob Zuma

Kulingana na gazeti la The Sunday Times, pesa hizo ziliwasilishwa kwake taslimu kwenye mifuko ya zawadi.

 
Msemaji wa Mamlaka ya Taifa ya Mashtaka amesema, msako huo ulifanywa na kurugenzi yake ya uchunguzi.
 
Mapisa-Nqakula alikuwa amepangiwa kuongoza kikao cha Bunge jana Jumanne ambapo wabunge waliuliza maswali kwa Rais Cyril Ramaphosa. Hata hivyo hakuhudhuria kikao hicho na zoezi hilo likasimamiwa na naibu wake.
 
Chama cha upinzani cha Democratic Alliance kimemtaka spika huyo ajiuzulu kwa hoja kwamba "hawezi kukabidhiwa afisi hiyo kuu."
 
Kabla ya hapo Bi Mapisa-Nqakula aliwahi kutuhumiwa kupokea rushwa alipokuwa waziri wa ulinzi, lakini uchunguzi wa bunge ulifutwa wakati alipochaguliwa kuwa Spika mwaka 2021.
 
Mapisa-Nqakula ni kiongozi mwingine mkuu wa ANC anayetuhumiwa kwa ufisadi wakati wa uongozi wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ambaye aliongoza nchi hiyo iliyoendelea zaidi barani Afrika kutoka 2009 hadi 2018 kabla ya kulazimishwa kujiuzulu kutokana na mlolongo wa tuhuma za ufisadi.../

 

Tags