Mar 24, 2024 07:03 UTC
  • Zaidi ya wanafunzi 200 waliokuwa wametekwa nyara Nigeria wameachiwa huru

Zaidi ya wanafunzi 200 pamoja na wafanyakazi waliokuwa wametekwa nyara na watu wenye silaha katika skuli moja kaskazini mwa Nigeria mapema mwezi huu wameachiliwa. Hayo ni kwa mujibu wa ofisi ya gavana wa jimbo la Kaduna lililoko kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Gavana wa Kaduna Uba Sani amesema leo Jumapili kwamba Mshauri wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo aliratibu kuachiliwa kwa watoto hao. Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi.
 
Sani ameongezea kwa kusema: "Jeshi la Nigeria pia linastahili pongezi maalumu kwa kuonyesha kwamba kwa ujasiri, azma thabiti na moyo wa kujitolea, wahalifu wanaweza kuangamizwa na usalama kurejeshwa katika jamii zetu".
Wanafunzi wakiwa darasani katika skuli ya msingi kaskazini ya Nigeria

Utekaji nyara huo, ambao ulifanyika mnamo Machi 7 katika mji wa Kuriga kaskazini magharibi mwa Jimbo la Kaduna, ulikuwa utekaji nyara wa kwanza wa umati mkubwa wa watu kufanywa nchini Nigeria tangu 2021.

 
Wiki iliyopita, watekaji nyara hao wenye silaha walidai kikomboleo cha jumla ya naira bilioni 1 ($690,000) kwa ajili ya kuwaachilia huru watoto na wafanyakazi waliopotea.
 
Utekaji nyara unaofanywa na magenge ya wahalifu yanayodai fidia, ambayo hayana mfungamano na makundi yenye itikadi kali, umekuwa sehemu ya matukio ya kila siku, hususan kaskazini mwa Nigeria, yanayosambaratisha familia na jamii zinazolazimika kukusanya akiba zao ili kulipa fidia, mara nyingi kwa kuuza ardhi, ng'ombe na nafaka, ili kuhakikisha wapendwa wao wanaachiwa huru na kubaki salama.../

 

Tags