Mar 31, 2024 11:41 UTC
  • Ukame uliokithiri kusini mwa Afrika umewasababishia njaa mamilioni ya watu

Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umetangaza kuwa ukame ulioziathiri Zimbabwe na majirani zake Zambia na Malawi umefikia viwango vya hatari. Zambia na Malawi tayari zimetangaza kuwa zinakabiliwa na majanga ya kitaifa. Ukame pia umeiathiri Msumbiji na Madagascar kwa upande wa mashariki.

Mwaka uliopita maeneo mengi ya kusini mwa bara la Afrika yalikumbwa na dhoruba kali za kitropiki na mafuriko. Ni mabadiliko ya hali ya hewa ambayo wanasayansi wanasema yanazidi kuongezeka na kusababisha uharibifu mkubwa zaidi kwa watu walio katika mazingira hatarishi. 

Shirika la WFP limesema kuwa limekusudia kutoa msaada kwa watu milioni 2.7 katika maeneo ya vijijini huko Zimbabwe ambao wanatishiwa na njaa kwa sababu ya ukame ulioyaathiri maeneo mengi ya kusini mwa bara la Afrika tangu mwaka jana. 

Raia wa Zimbabwe kwa jina la Ncube amesema kuwa na hapa ninamnukuu "Hatuna chochote mashambani, hata nafaka moja,” Kila kitu kimeteketezwa na ukame."

Ukame ulivyoathiri mazao ya nafaka nchini Zimbabwe 

Wakati huo huo Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umeeleza kuwa kuna majanga yanayoingiliana ya hali mbaya ya hewa mashariki na kusini mwa Afrika, ambapo mwaka jana maeneo hayo mawili yaliathiriwa na dhoruba, mafuriko, joto na ukame.

Unicef imeongeza kuwa huko kusini mwa Afrika, wastani wa watu milioni 9, nusu yao wakiwa ni watoto, wanahitaji msaada huko Malawi. Aidha watu zaidi ya milioni 6 huko Zambia, milioni 3 kati yao wakiwa ni watoto wameathiriwa na ukame.

 

Tags