Apr 19, 2024 04:43 UTC
  • Mkuu wa Majeshi na makamanda tisa waandamizi wa Kenya wafariki katika ajali ya helikopta

Kenya inaomboleza kifo cha Mkuu wa Majeshi (KDF), Jenerali Francis Omondi Ogolla ambaye ameaga dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea jana Alkhamisi katika eneo la Sindar kwenye mpaka wa Kaunti ya Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet.

Jenerali Ogolla alifariki dunia pamoja na maafisa wengine tisa waandamizi wa jeshi la Kenya waliokuwemo ndani ya helikopta ya KDF iliyokuwa na maafisa wengine 11 wa jeshi hilo wakati ajali hiyo ilipotokea dakika chache baada ya saa tisa alasiri.

Rais William Ruto ametangaza siku tatu za kumuombeleza Jenerali Ogolla na maafisa wengine waliofariki wakiwa kazini.

Rais Ruto aliliambia taifa akiandamana na makamanda wakuu wa KDF na waziri wa Ulinzi Aden Duale katika Ikulu ya Nairobi: "ni siku ya huzuni. Leo nchi yetu imekumbwa na ajali mbaya iliyomuua Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Jenerali Francis Omondi Ogolla”.

Maafisa hao walikuwa wakitoka katika ziara ya kikazi katika shule ya sekondari ya wavulana ya Cheptulel, Pokot Magharibi ambako walihudhuria mkutano kwa saa moja.

Rais Ruto amesema, Jenerali Ogolla na maafisa wake walikuwa wametembelea wanajeshi wanaosaidia katika vita dhidi ya ujangili katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Tito Lopuriang, mkazi wa eneo la Cheptulel alilotembelea Jenerali Ogolla na maafisa wenzake amesema, baada ya mkutano na machifu wa eneo hilo na maafisa wengine wa utawala mkuu huyo wa Majeshi ya Kenya na wenzake walipanda helikopta ya jeshi aina ya buffalo iliyooondoka dakika chache kabla ya saa tisa na dakika chache baadaye, wakazi wakaona moshi baada ya helikopta hiyo kuanguka eneo la Sindar upande wa Marakwet, takriban kilomita mbili kutoka Chesegon.

Kamishna wa Kaunti ya Pokot Magharibi Khalif Abdullahi alithibitisha kuwa helikopta hiyo ilianguka katika mpaka wa kaunti hiyo na Elgeyo Marakwet.

Jenerali Ogolla aliteuliwa mkuu wa majeshi ya ulinzi ya Kenya mnamo Aprili 28, 2023 baada ya kustaafu kwa Jenerali Robert Kibochi mnamo Aprili 28, 2023.../

 

Tags