Apr 20, 2024 02:57 UTC
  • Afrika, mhanga mkubwa zaidi wa mabadiliko ya hali ya hewa, ingawa haichangii sana katika kuyaanzisha

Uchunguzi unaonyesha kuwa, Bara la Afrika ndilo lililo hatarini zaidi kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi katika hali zote za hewa licha ya kwamba Afrika haichangii isipokuwa asilimia ndogo sana ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Ripoti zinaonyesha kuwa, licha ya mchango wake mdogo katika ongezeko la joto duniani, bara la Afrika linakabiliwa na hatari kubwa kwa uchumi wake na uwekezaji katika miundombinu, mifumo ya maji, chakula, afya ya umma, kilimo na maisha kutokana na mabadiliko ya tabianchi. 

Afrika inaathiriwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa

Afrika ina nchi 17 kati ya 20 zilizo hatarini zaidi kutokana na vitisho vya hali ya hewa kote ulimwenguni, na mabadiliko ya hali ya hewa tayari yanaathiri kati ya asilimia 2 na 9 ya bajeti ya kitaifa katika bara zima la Afrika, na kutishia kuziingiza katika viwango vya juu vya umaskini uliokithiri, kuchochea uhamaji na ukimbizi, na kuongeza hatari ya migogoro na mapigano ya kugombania rasilimali zinazoendelea kupungua.

Ripoti ya Hali ya Hewa barani Afrika 2022 inaonyesha kuwa kasi ya ongezeko la joto barani humo imeongezeka katika miongo ya hivi karibuni huku hali ya hewa na hatari zinazohusiana na hali ya hewa zikizidi kuwa mbaya.

Zaidi ya watu milioni 110 waliathiriwa moja kwa moja na hali ya hewa, mazingira na maji mnamo 2022, na kusababisha uharibifu wa kiuchumi wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 8.5 na zaidi ya vifo vya watu 5,000, ambapo 48% vilihusiana na ukame na 43% vilihusiana na mafuriko.

Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa hasara ya Pato la Taifa katika nchi za Afrika itaongezeka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, na ongezeko la nyuzi joto 2 la joto duniani litawaweka zaidi ya nusu ya wakazi wa bara hilo kwenye hatari ya utapiamlo.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, bara la Afrika - ambalo lina takriban 17% ya idadi ya watu duniani - linawakilisha sehemu ndogo zaidi ya uzalishaji wa gesi chafu kwenye sayari ya dunia kwa 3.8% tu, ikilinganishwa na karibu 23% nchini China na 19% nchini Marekani.