Apr 21, 2024 11:35 UTC
  • Mauzo ya bidhaa za Russia barani Afrika ni zaidi ya mauzo Amerika

Bara la Afrika limeongeza kwa kiasi kikubwa uagizaji wa bidhaa kutoka Russia, na kuwashinda washirika wa kibiashara wa Moscow kutoka Amerika ya Kaskazini na Kusini. Hayo ni kwa mujibu wa data za kiuchumi zilizochapishwa na gazeti la kila siku la biashara la RBK nchini Russia.

Gazeti hilo limenukulu ripoti ya Huduma ya Forodha ya Shirikisho la Russia (FCS) ikionyesha kuwa mwaka uliopita wa 2023, mchango wa bidhaa za Kiafrika katika mauzo ya nje ya Russia uliongezeka kwa asilimia 100.

Wakati huo huo, mchango wa  eneo kubwa la  bara Amerika, ambayo ni pamoja na Karibiani, Amerika ya Kati, Amerika Kusini na Amerika Kaskazini, umeripotiwa kupungua kwa asilimia 2.9 mwaka huo.

 Mauzo ya nje ya Russia  kwa mataifa ya Afrika yaliongezeka na kufikia dola bilioni 21.2, wakati mauzo kwa nchi za Amerika Kaskazini na Kusini yalipungua kwa asilimia 40 na kufika billioni 12.2.

Gazeti la RBK pia liliandika kwamba mwaka 2023, mauzo ya bidhaa za petroli za Russia kwenda Afrika  yaliongezeka karibu maradufu, huku mauzo ya ngano pia yakiongezeka kwa kiasi kikubwa.

Katika miaka ya hivi karibuni nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikijikurubisha zaidi kwa Russia katika sekta za kiuchumi na kisiasa baada ya kuchoshwa na sera za kibeberu za nchi za Magharibi.