Apr 23, 2024 12:19 UTC
  • UN: Mapigano yamewalazimisha watu 50,000 kukimbia makazi yao kaskazini mwa Ethiopia

Umoja wa Mataifa umefichua kuwa zaidi ya watu 50,000 wamekimbia makazi yao kaskazini mwa Ethiopia, kutokana na mapigano yanayojiri katika eneo linalozozaniwa kati ya majimbo ya Tigray na Amhara. Mapigano ya pande hizo mbilii yamezua wasiwasi wa kimataifa.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema katika ripoti iliyochapishwa jana usiku kwamba "idadi ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano ya silaha katika mji wa Raya Alamata tangu Aprili 13 imepita watu 50,000."

OCHA imeripoti kwamba, takriban watu 42,000 waliokimbia makazi yao wamekimbia kuelekea kusini, haswa karibu na mji wa Kobo, na 8,300 wameelekea mji wa Sekota kaskazini. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa wengi kati ya waliokimbia makazi yao ni "wanawake, watoto, vijana na wazee".

Alamata na viunga vyake viko katika eneo linalozozaniwa la Raya kati ya Tigray na Amhara, ambapo mapigano yalizuka kati ya wapiganaji wa makabila hayo mawili takriban siku 10 zilizopita.

Jumamosi iliyopita, balozi za nchi za kigeni nchini Ethiopia, zilieleza "wasiwasi wao juu ya ripoti za ghasia katika maeneo yanayozozaniwa kaskazini mwa Ethiopia," na kutoa taarifa ya pamoja ya wito wa "komeshwa ongezeko la machafuko na kulindwa raia."