May 01, 2024 05:13 UTC
  • Rwanda yatahadharisha: Mito huenda ikavunja kingo zake, nchi za kanda zaendelea kuathiriwa

Rwanda, imetangaza kwamba kutokana na mvua kubwa iliyotabiriwa katika wiki ya kwanza ya Mei, baadhi ya mito inaweza kuvunja kingo zake na kusababisha mafuriko katika jamii.

Tahadhari hiyo ilitolewa jana Jumanne na Bodi ya Rasilimali za Maji ya Rwanda (RWB), na kusisitiza kuwa, mito inayoweza kusababisha mafuriko ni pamoja na Mto Sebeya, Karambo, Nyabahanga, Kabirizi, Nyabarongo, Mwogo, Mukungwa, Rubyiro, Cyagara, pamoja na mito ya Ukanda wa Virunga.

Bodi hiyo imewataka watu wanaoishi karibu na mito hiyo kuhama maeneo hayo na kuepuke maeneo hatarishi.

Mvua kubwa za msimu huu tayari zimesababisha maafa nchini Rwanda na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki hususan Kenya na Tanzania. Zaidi ya watu mia tatu wameripotiwa kufarikki dunia katika nchi hizo mbili kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa. 

Mvua kubwa iliyosababishwa na El Niño na mafuriko vinaendelea kuathiri sehemu za ukanda wa Afrika Mashariki, zikiwemo Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini na Sudan.