May 07, 2024 02:16 UTC
  • SADC kutekeleza mashambulizi ya 'kuwamaliza' waasi wa M23 DRC

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) imetangaza kuwa, vikosi vyake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vitafanya mashambulizi, kwa ushirikiano na vikosi vya serikali, ili "kuwamaliza waasi wa M23 na kurejesha amani na usalama."

SADC imetangaza hayo katika taarifa yake ikilaani shambulio la bomu dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Mugunga nje kidogo ya mji wa Goma, ambalo inasema lilitekelezwa na waasi wa M23. Taarifa zinasema, shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu takriban 16 na kujeruhi wengine takriban 30.

Kundi la waasi wa M23 limekanusha vikali madai hayo. Gavana wa Jimbo la Kivu, Ruguru, alisema kuwa watu 14 walifariki na wengine zaidi ya 35 kujeruhiwa katika shambulio la kambi ya Mugunga.

Vikosi vya SADC vimekuwa Kivu Kaskazini tangu mwishoni mwa mwaka jana na tangu Januari mwaka huu vimeshiriki katika makabiliano ya "moja kwa amoja" dhidi ya M23 kwa kutumia "mizinga mizito, ndege za kivita, ndege zisizo na rubani, na vifaru" katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa M23.

Waasi wa M23 wamehatarisha usalama katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

 

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo, ilialika kikosi hicho cha SADC baada ya kusema kuwa haijaridhika na wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ambao walitakiwa kupambana na waasi wa M23.

Kongo DR imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.