Ethiopia yahamakishwa na EU kuiwekea vizuizi katika upokeaji wa viza
Ethiopia imeeleza kughadhabishwa na hatua ya Baraza la Umoja wa Ulaya ya kuwawekea raia wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika vikwazo na vizingiti katika upokeaji wa viza.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia, Nebiyu Tedla amewaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa kuwa, serikali ya nchi hiyo italiandikia barua Baraza la EU kulitaka liangalie upya vizingiti hivyo visivyo vya kiadilifu dhidi ya taifa hilo.
Aprili 29, Baraza la EU liliamua kurefusha muda wa kushughulikia mchakato wa utoaji viza kwa wananchi wa Ethiopia kutoka siku 15 hadi 45, likidai kuwa Addis Ababa imekataa kusaidia katika mpango wa kuwarejesha nyumbani Waethiopia wanaoishi kinyume cha sheria katika nchi za Ulaya.
Aidha uamuzi huo wa Baraza la EU unamaanisha kuwa, Waethiopia sasa hawataweza kupewa viza za kuingia mara kadhaa katika nchi za Ulaya, na pia wanadiplomasia wa nchi hiyo ya Kiafrika watalazmika sasa kulipia kibali hicho muhimu cha kusafiria.
Hitilafu kuhusu kadhia ya wahamiaji miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya zingali zinaendelea licha ya makubaliano ya hivi karibuni kuhusu suala hilo. Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa EU karibuni alitahadharisha kuwa umoja huo umegawanyika pakubwa kuhusu zera za uhamiaji na kuwa suala hilo linaweza kupelekea kuvunjika umoja huo.
Kadhalika Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ethiopia amekosoa taarifa ya pamoja iliyotolewa karibuni na balozi Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Sweden, na Australia, ikidai kuwa baadhi ya nyakati waandishi wa habari nchini Ethiopia wanatishiwa na kuzuiliwa kwa 'kufanya kazi yao'.