May 25, 2024 07:22 UTC
  • Afrika Kusini yataka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liwalinde Wapalestina

Afrika Kusini siku ya Ijumaa ilisema kwamba inafuatilia kuona jinsi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakavyojibu uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wa kuuamuru utawala wa Israel usitishe mara moja mashambulizi yake ya kijeshi huko Rafah, mji ulioko kusini mwa Ukanda wa Gaza ambako ulituma vikosi mnamo Mei 6.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naledi Pandor aliliambia shirika la habari la SABC Ijumaa kwamba: "Tuna furaha kwamba mahakama imezingatia kwa uzito masuala ambayo tuliwasilisha mbele yake na imethibitisha kwamba uamuzi wa haraka unahitajika kutoka kwa mahakama hiyo ili kusitisha mashambulizi haya dhidi ya Wapalestina wasio na hatia,"

Pandor amesema Israel imekuwa "ikikiuka sheria bila kujali kwa muda mrefu" kiasi kwamba haijali kile ambacho jumuiya ya kimataifa inasema.

Naledi Pandor

Ameongeza kuwa: "Nadhani ni jukumu letu kama nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa sababu ndilo lenye jukumu la kusimamia Amani na Usalama duniani kwa hivyo sasa lazima waamue hatua zitakazochukuliwa kuwalinda watu wa Palestina."

Amesema uamuzi wa mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa ni "wito wa wazi kabisa" wa kusitisha mashambulizi dhidi ya Rafah.

Pandor amesema kumekuwa na mwamko wa kimataifa kuhusu hali ya Palestina na nchi tajiri za kaskazini sasa zinaanza kuzungumza dhidi ya ukatili wa Israel na kuitambua Palestina.