Watu 10 wameuawa Nairobi wakati polisi ilipowafyatulia risasi waandamanaji waliovamia bunge
Watu 10 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa jana Jumanne wakati polisi walipowafyatulia risasi mamia ya waandamanaji waliovamia majengo ya bunge jijini Nairobi, mji mkuu wa Kenya, kupinga sheria ya iliyopitishwa na wabunge ya kuongeza ushuru.
Mfanyakazi mmoja wa kujitolea wa Taasisi ya Msalaba Mwekundu ambaye alizungumza na Shirka lal habari la Anadolu kwa sharti la kutotajwa jina alisema kuwa takriban watu 10 waliuawa, huku idadi ya vifo ikitazamiwa kuongezeka huku majeruhi kadhaa wakiendelea kupatiwa matibabu kutokana na majeraha ya risasi.
Katika hali ya taharuki, waandamanaji walionekana ndani ya ukumbi wa Bunge mjini Nairobi wakiwa wamesimama juu ya kiti cha spika. Vijana waliokuwa na hasira pia walichoma moto sehemu za bunge na ofisi ya gavana wa Nairobi.
Wabunge wa Kenya jana walilazimika kutafuta hifadhi katika njia ya chini ya ardhi wakati waaandamanaji walipovamia jengo la bunge. Baadhi ya ripoti zimearifu kuwa waandamanaji wameiba na kupora mali katika baadhi ya maduka na biashara za watu katika maeneo mbalimbali ya Kenya.