Wataalamu: Eneo huria la biashara barani Afrika litachochea ukuaji wa biashara jumuishi
Wataalamu wa Kiafrika walisema jana Jumatatu huko Nairobi Kenya kwamba utekelezaji kamili wa Eneo Huria la Biashara barani Afrika (AfCFTA) utaleta ukuaji shirikishi katika bara zima.
Wakizungumza katika Mkutano wa kila mwaka wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB huko Nairobi, Kenya, wataalamu hao wamesema kuwa bara la Afrika litapunguza kutegemea masoko ya jadi ya magharibi iwapo biashara zitaongezeka katika bara hilo.
Vincent Nmehielle Katibu Mkuu wa kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika amesema kuwa kuendesha biashara huria barani Afrika kwa kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya bara hilo kutakuza biashara ya ndani ya Afrika, na wakati huo huo kunufaisha wafanyabiashara wadogo.
John Bosco Kalisa Afisa Mtendaji mkuu wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki ameeleza kuwa baraza hilo hivi sasa linatoa mafunzo kwa makampuni madogo na yale yanayomilikiwa na wanawake kuhusu taratibu za kufanya biashara chini ya usimamizi wa AfCFTA.
Naye Monale Tatsoma Mkurugenzi Mkuu wa Benki Mpya ya Maendeleo ya Afrika ya kundi la BRICS kanda ya Afrika taasisi yake inatoa kipaumbele kwa maendeleo ya miradi ya miundombinu barani Afrika ili kurahisisha biashara barani humo.