May 28, 2024 10:42 UTC
  • Mauritius yaungana na Afrika Kusini katika mashtaka dhidi ya utawala wa Israel

Serikali ya Mauritius metangaza kuungana na mashtaka ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaofanya mauaji katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Msimamo huo wa Mauritius umetangazwa na Mohammad Anwar Husnoo Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo ambaye amesisitiza kuwa, nchi yake inapinga vikali mauaji ya kinyama yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.

Mohammad Anwar Husnoo sambamba na kuunga mkono uamuzi wa Afrika Kusini wa kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel amesema kuwa, ana matumaini jamii ya kimataifa  itachukua hatua madhubuti ili kusitishwa hujuma na mashambulio ya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Tarehe 29 Disemba mwaka jana (2023), Afrika Kusini iliwasilisha kesi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague Uholanzi ikiutuhumu utawala huo wa Kizayuni kwa kukiuka Makubaliano ya Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1948 wakati wa operesheni zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza.

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ)

 

Katika mashtaka yake, Afrika Kusini inaushutumu utawala wa Kizayuni kwa vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. Mnamo Januari, Mahakama ya ICJ iliamuru Israel ihakikishe wanajeshi wake hawafanyi mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza, kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu na kuhifadhi ushahidi wowote wa ukiukaji wa hatua hizo, lakini utawala huo haujatekeleza agizo hata moja la mahakama hiyo.

Tags