Rwanda: Hatutamkamata Rais al-Bashir wa Sudan akija nchini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11266-rwanda_hatutamkamata_rais_al_bashir_wa_sudan_akija_nchini
Rwanda imesema itamkaribisha Rais Omar al-Bashir wa Sudan atakapoizuru nchi hiyo kesho Jumamosi kuhudhuria kongamano Umoja wa Afrika AU, licha ya kiongozi huyo kuandamwa na waranti wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC wa kutaka akamatwe.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2016 23:42 UTC
  • Rwanda: Hatutamkamata Rais al-Bashir wa Sudan akija nchini

Rwanda imesema itamkaribisha Rais Omar al-Bashir wa Sudan atakapoizuru nchi hiyo kesho Jumamosi kuhudhuria kongamano Umoja wa Afrika AU, licha ya kiongozi huyo kuandamwa na waranti wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC wa kutaka akamatwe.

Katika kikao na waandishi wa habari mjini Kigali jana Alkhamisi, Bi Louise Mushikiwabo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Rwanda amesema, nchi hiyo haitamkamata Rais al-Bashir na wala haitomkabidhi kwa mahakama ya ICC kwa kuwa mahakama hiyo 'imegubikwa na siasa.'

Aidha ameikosoa vikali mahakama hiyo ya kimataifa kwa kile alichokitaja kwamba, imekuwa ikitumika kuwaandama viongozi wa bara la Afrika tu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda amesema, Rais Bashir anaenda Kigali kushiriki kongamano la viongozi wa Umoja wa Afrika na moja ya ajenda za mkutano huo ni kujadili uwezekano wa nchi za Kiafrika kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliobuni ICC na kuandaa mazingira ya kubuniwa mahakama ya kieneo. Hata hivyo Rwanda si mwanachama wa Mkataba wa Roma.

Jumanne iliyopita, mahakama ya ICC ilizishtaki Uganda na Djibouti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa kushindwa kumkamata rais huyo wa Sudan alipofanya ziara katika nchi hizo hivi karibuni. ICC ilitoa waranti wa kumkamata Rais al Bashir mwaka 2009 na mwaka 2010, kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu uliotokea mkoani Darfur, magharibi mwa Sudan.