Jeshi la Uganda lakanusha madai ya kuwaunga mkono waasi wa M23
(last modified Tue, 18 Jun 2024 02:41:00 GMT )
Jun 18, 2024 02:41 UTC
  • Jeshi la Uganda lakanusha madai ya kuwaunga mkono waasi wa M23

Jeshi la Uganda (UPDF) limekanusha madai kwamba linatoa msaada kwa wapiganaji wa M23 ambao wanaendesha harakati zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kanusho hilo limetolewa na naibu msemaji wa jeshi la Uganda Luteni Kanali Deo Akiiki ambaye ameitaja ripoti iliyotolewa na kundi maalumu la wataalamu wa Umoja Mataifa kuwa, ya upotoshaji na  kuonyesha uzembe katika kufanya uchunguzi bila kufuatilia hali halisi ya mambo.

Madai hayo yametolewa wakati wimbi jipya la mzozo likifukuta mashariki mwa Congo ambapo zaidi ya raia 150 wameuawa katika mashambulizi yanayofanywa na waasi wa ADF  katika kipindi cha mwezi mmoja.

Wiki iliyopita, ripoti hiyo kuhusiana na amani na usalama mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ilielezea kuwa Uganda inatoa msaada kwa wapiganaji wa M23 pamoja na kundi lingine lijulikanao kama Alliance Fleuve Congo (AFC).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, licha ya wapiganaji wa M23 kuwekewa vikwazo na Umoja Mataifa, lakiini Uganda imewaruhusu viongozi wao husafiri nchi za nje wakipitia uwanja wa kimataifa wa Entebbe.

Mapigano makali kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali yamesababisha wimbi jipya la wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Duru mbalimbali katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini zimeripoti kuhusiana na wimbi hilo jipya la wakimbizi.

Mwezi Januari mwaka huu Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilitangaza kuanzisha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya Maendelezo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC dhidi ya waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.