Jul 10, 2024 12:21 UTC
  • Mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini yanakabiliwa na hatari ya kuvunjika

Mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa yanakaribia kukamilika, yamekumbwa na mkwamo baada ya makundi ya upinzani ya nchi hiyo kutaka kufutwa kwa muswada mpya uliopasishwa unaoruhusu kuwekwa kizuizini watu bila kwanza kutolewa hati ya kukamatwa.

Makundi hayo ya upinzani yamesema kuwa muswada huo mpya unapasa kufutwa ili waweze kutia saini makubaliano yaliyopendekezwa.

Kenya imekuwa mwenyeji wa mikutano ya ngazi ya juu ya mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini tangu mwezi Mei mwaka huu kati ya wawakilishi wa serikali na makundi ya waasi ambayo hayakuwa sehemu ya makubaliano ya 2018 yaliyohitimisha vita vya ndani vya miaka mitano nchini humo.

Vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe viliuwa watu wasiopungua 400,000 na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Mapigano na ghasia zimekuwa zikishuhudiwa mara kwa mara huko Sudan Kusini, nchi iliyo na jamii ya watu milioni 9 licha ya kufikiwa mapatano ya amani. 

Pagan Amum Okiech Mwakilishi wa kundi la upinzani la South Sudan Opposition Movement Alliance katika mazungumzo ya sasa ya amani ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa hakuna maana kutia saini makubaliano iwapo Sheria ya Usalama wa Taifa itatiwa saini na rais kuwa sheria."

Pagan Amum Okiech 

Wiki jana, Bunge la Sudan Kusini lilipiga kura na kuunga mkono muswada wa  2015, na Rais wa nchi hiyo Salva Kiir anatakiwa kuupasisha katika muda wa sku 30 ili kuwa sheria. Hatua hii imejiri kabla ya kufanyika uchaguzi wa kwanza huko Sudan Kusini Disemba 22 mwaka huu. 

Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch pia limemtaka Rais Kiir kuutupilia mbali muswada huo wenye utata likisema kuwa utadhoofisha zaidi haki za binadamu huko Sudan Kusini na kuvipa nguvu idara za usalama wa taifa ambazo zina historia ya muda mrefu ya kukiuka haki za binadamu.

Tags