Mandela: Houthi wazidishe mashambulizi ili kuikomboa Palestina
(last modified Mon, 22 Jul 2024 10:58:52 GMT )
Jul 22, 2024 10:58 UTC
  • Mandela: Houthi wazidishe mashambulizi ili kuikomboa Palestina

Mjukuu wa Nelson Mandela, shujaa na kiongozi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini ametoa mwito kwa Harakati ya Ansarullah na vikosi vya wanajeshi wa Yemen kushadidisha operesheni zao dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaoendelea kuua watoto na wanawake wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza.

Nkosi Zwelivelile Mandela, ambaye ni mbunge katika Bunge la Afrika Kusini ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la Russia Today na kueleza kuwa: Tunasema kama harakati za kimataifa za kuonyesha mshikamano (na Palestina) kuwa, Mahouthi (wanaharakati wa Ansarullah) wanapasa kusimama kidete na kuzidisha vita vya kuwakomboa mandugu na madada zetu wa Gaza na maeneo mengine yote ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Operesheni za majeshi ya Yemen za kuwaunga mkono wananchi madhulumu Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, zimekuwa na mafanikio makubwa na zinaendelea kuisababishia Israel hasara zisizo na kifani.

Kadhalika mjukuu wa Nelson Mandela ametoa mwito wa kuwepo harakati za kimataifa za kuharakisha suala la ukombozi wa Palestina; sambamba na kupigwa marufuku utawala haramu wa Israel kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.

"Mandla" Mandela amesema Wapalestina zaidi ya 400 waliopaswa kushiriki mashindano hayo ya kimataifa huko Ufaransa wameuawa pamoja na wakufunzi wao kwa mabomu ya Wazayuni.

"Sisi waungaji mkono wa Palestina, leo tuko hapa Paris kutoa mwito kwa jamii yote ya kimataifa kushinikiza kupigwa marufuku utawala wa apartheid wa Israel kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris," amesisitiza Mandela.