Baraza la Usalama laidhinisha MONUSCO kuipa SADC msaada wa kilojistiki DRC
(last modified Wed, 07 Aug 2024 06:43:58 GMT )
Aug 07, 2024 06:43 UTC
  • Baraza la Usalama laidhinisha MONUSCO kuipa SADC msaada wa kilojistiki DRC

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la kuidhinisha kikosi cha kusimamia amani cha umoja huo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo MONUSCO kutoa msaada wa kiutendaji na wa suhula na zana za kijeshi kwa ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) nchini DRC.

Rasimu ya azimio hilo iliyowasilishwa na Ufaransa na Sierra Leone, ilipigiwa kura jana Jumanne katika Baraza la Usalama lenye wanachama 15, na kupitishwa kwa kauli moja.

Akizungumza kabla ya upigaji kura, Mwakilishi wa Kudumu wa Sierra Leone katika Umoja wa Mataifa, Michael Imran Kanu, amesema azimio hilo "linalenga kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa juhudi za amani za kikanda."

Amebainisha kuwa azimio hilo "linasisitiza umuhimu wa kulindwa raia, kuhakikisha uratibu madhubuti, na ushirikiano mzuri kati ya MONUSCO, SADC na Ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo SAMIDRC."

Wakongomani wamekuwa wakiandamana wakitaka kufukuzwa nchini humo askari wa UN

Azimio hilo limepasishwa wiki chache baada ya kikosi cha MONUSCO kufungasha virago vyake na kuondoka Kivu Kusini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa ombi la serikali ya Kinshasa. MONUSCO ilianza kusitisha shughuli zake huko Kivu Kusini Januari mwaka huu.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mwanzoni mwa mwaka huu ilialika kikosi cha SADC baada ya kusema kuwa haijaridhika na wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ambao walitakiwa kupambana na waasi wa M23 mashariki mwa nchi.