Upinzani Kongo wataka kuchukuliwa hatua kuzuia mabadiliko ya katiba
Vyama vya upinzani nchini Jamhuri ya Kidmemokrasia ya Kongo vimewatolea wito wananchi kupinga mipango tarajiwa inayoandaliwa na Rais Felix Tshisekedi wa nchi hiyo ya kubadilisha katiba.
Chama tawala nchini humo mwezi Oktoba kiliwataka wanachama wake kushughulikia suala la kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo; ambapo vyama vya upinzani vinahofia kuwa mabadiliko yatakayotekelezwa yanaweza kurefusha muda wa kusalia madarakani Rais Tshisekedi.
"Wakongo, hali hii ni mbaya, amkeni! Tutetee haki zetu na uhuru wetu," amesema Devos Kitoko Katibu Mkuu wa chama kinachoongozwa na Martin Fayulu ambaye ni miongoni mwa wapinzani wakuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Itakumbukwa kuwa Rais Felix Tshisekedi mwezi Oktoba mwaka huu alitangaza mipango ya kuunda kamisheni ya kuchunguza marekebisho ya katiba.