Ushirikiano wa Togo na Burkina Faso katika vita dhidi ya ugaidi
Nchi mbili za magharibi mwa Afrika za Togo na Burkina Faso zimesisitizia wajibu wa kushirikiana katika kupambana na ugaidi kwenye eneo lao.
Yark Damehame, Waziri wa Usalama wa Togo na Simon Compaore, waziri mwenzake wa Burkina Faso wamekutana katika mji wa Dapaong wa kaskazini mwa Lome, mji mkuu wa Togo kwa ajili ya kujadiliana namna ya kuimarisha usalama wa eneo hilo na jinsi nchi zao zinavyoweza kushirikiana katika vita dhidi ya ugaidi. Viongozi wa Togo na Burkina Faso wamesisitizia pia haja ya kubadilishana taarifa za kijasusi kwa ajili ya kupambana na vitendo hivyo vya kigaidi. Togo na Burkina Faso ni wanachama wa jumuiya ya Sahel ambayo ilianzishwa mwaka 1998 mjini Tripoli, Libya. Jukumu la jumuiya hiyo ni kulinda usalama na amani pamoja na kudumisha utulivu kwenye nchi za eneo hilo. Katika hati ya kuunda jumuiya hiyo imeandikwa kuwa, kazi ya kulinda usalama wa nchi wanachama, lazima ifanyike kwa njia ya mazungumzo ya kisiasa na kupambana na ugaidi. Mashambulizi ya kigaidi katika nchi za Mali, Burkina Faso na Kodivaa yamepelekea wakuu wa eneo hilo kufikiria suala la kuimarisha ushirikiano wao katika vita dhidi ya ugaidi. Rais Mahamadou Issoufou wa Niger ametoa mwito wa kuundwa kikosi cha pamoja na kieneo huko magharibi mwa Afrika kwa ajili ya kupambana na ugaidi. Alitoa mwito huo kwenye kikao cha "Baraza la Fikra za Pamoja" la magharibi mwa Afrika, kilichofanyika Niamey, mji mkuu wa Niger. Alisisitiza kuwa, ni jambo la dharura kuundwa jeshi la nchi kadhaa za Afrika kama lile la nchi zinazopakana na Ziwa Chad. "Baraza la Fikra za Pamoja" lina wanachama watano ambao ni Niger, Kodivaa, Burkina Faso, Togo na Benin. Aidha Rais Mahamadou Issoufou wa Niger amesisitiza kuwa, vitisho vya mashambulizi ya kigaidi bado vipo na ni jambo la dharura kulipa uzito mkubwa suala la kupambana na vitendo hivyo. Genge la kigaidi la ISIS yaani Daesh linafanya jinai za kila namna nchini Libya na hilo ni tishio kubwa kwa nchi wanachama wa jumuiya ya Sahel. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana kikao kilichomalizika jana (Jumatatu, Julai 18, 2016) huko Kigali, mji mkuu wa Rwanda, cha wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, kikalipa umuhimu mkubwa suala la kupambana na ugaidi. Katika mkutano huo wa AU wa mjini Kigali, viongozi wa Afrika wametoa mwito wa kutengwa bajeti maalumu kwa ajili ya kupambana na ugaidi. Rais Idris Deby wa Chad ambaye nchi yake ndiye mwenyekiti wa hivi sasa wa Umoja wa Afrika, amewataka wakuu wa nchi walioshiriki kwenye mkutano wa Kigali, kulipa kipaumbele kikuu suala la kupambana na ugaidi. Amesema, kuanzisha mfuko maalumu wa kupambana na ugaidi barani Afrika ni jambo la dharura mno na kwamba fedha za mfuko huo inabidi zitolewe na nchi zenyewe za Afrika wanachama wa AU na sio kusubiri misaada kutoka nje. Naam, ni jambo lisilo na shaka kuwa ugaidi ni tishio kubwa si barani Afrika pekee, lakini duniani nzima, na ushirikiano wa kweli unahitajika kwa ajili ya kupambana na vitendo vya kigaidi bila ya kuingiza misimamo ya kindumakuwili katika jambo hilo muhimu sana.