UN: Mafuriko yawaathiri maelfu ya watu magharibi na katikati mwa Afrika
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeripoti kuwa watu zaidi ya 700,000 wameathiriwa na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabianchi mwaka huu huko magharibi na katikati mwa Afrika.
Mafuriko yameharibu na kubomoa nyumba zaidi ya elfu sitini na kuwaacha watu zaidi ya 54,000 yaani wanawake, watoto na wanaume bila ya makazi. Mafuriko hayo pia yamesababisha maafa na hasara kwa shule na vituo vya matibabu.
Ofisi ya OCHA imeongeza kuwa watu wasiopungua 72 wameaga dunia kwa kuzama majini na wengine karibu ya 700 wamejeruhiwa. Nchi zilizoathiriwa na mafuriko ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Cote d'ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Liberia, Niger, Nigeria, Mali na Togo.
Chad imeathirika pakubwa na mafuriko ambapo makazi ya watu zaidi ya 245,000 yamejaa maji.
Utabiri wa msimu wa 2024 ulitabiri mvua nyingi zaidi ya juu ya wastani kuanzia Juni hadi Agosti na Julai hadi Septemba mwaka huu katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko katika eneo la Sahel na baadhi ya nchi za Afrika Magharibi.