Rwanda yatia saini makubaliano ya ujenzi wa vinu vya nyuklia
Rwanda imetangaza kuwa, imetia saini mkataba wa maelewano na kampuni ya Kimarekani ya Nano Nuclear Energy kwa ajili ya ujenzi wa vinu vidogo vya nyuklia (SMR). Tangazo hilo limetolewa na Mamlaka ya Nishati ya Atomiki ya Rwanda (RAEB).
SMR ambavyo ni vinu vidogo na rahisi zaidi katika ujenzi kuliko mitambo ya kawaida ya nyuklia, vinazalishwa kwa wingi katika viwanda na kisha kusafirishwa hadi kwenye eneo vitakavyowekwa. Lengo la mkataba huu wa itifaki "ni kuanzisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili ili kuwezesha kuanzishwa kwa vinu vidogo", kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari kutoka RAEB.
Akiwa safarini nchini Rwanda, Mkurugenzi Mtendaji wa Nano Nuclear Energy, James Walker, ametangaza kwamba, ujenzi wa kinu cha majaribio utafanyika "katika miaka michache ijayo".
Aidha amesema kuwa, "Tuna msingi mzuri tunaozingatia, tunaona njia rahisi sana kuelekea mpango wa nyuklia wa kiraia unaoendelea nchini Rwanda," amesema, akinukuliwa katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Mkurugenzi wa RAEB Fidele Ndahayo alikaribisha hatii hiyo ya maelewano akisema kuwa, "Teknolojia za SMR kwa sasa ziko chini ya maendeleo na Rwanda inataka kuwa sehemu ya mchakato wa maendeleo." Rwanda, nchi ndogo isiyo na bahari katika eneo la Maziwa Makuu yenye wakazi wapatao milioni 13, inazalisha zaidi ya nusu ya umeme wake (51%) kutoka vyanzo vya joto, mbele ya umeme wa maji (43.9%) na jua (4.2%).
Mnamo mwezi Septemba 2023, mamlaka ya Kigali ilitia saini makubaliano na shirika la Ujerumani na Canada la Dual Fluid Energy ili kujenga kinu "majaribio" cha nyuklia ya kiraia.