Viongozi wa AU washindwa kuteua Kamishna Mkuu mpya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11542-viongozi_wa_au_washindwa_kuteua_kamishna_mkuu_mpya
Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) jana usiku walikamilisha mkutano wao wa siku mbili mjini Kigali, Rwanda bila ya kuweza kuchagua Kamishna Mkuu mpya wa umoja huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 19, 2016 03:30 UTC
  • Viongozi wa AU washindwa kuteua Kamishna Mkuu mpya

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) jana usiku walikamilisha mkutano wao wa siku mbili mjini Kigali, Rwanda bila ya kuweza kuchagua Kamishna Mkuu mpya wa umoja huo.

Viongozi wa Afrika walioshiriki mkutano wa Kigali walishindwa kuchagua mtu atakayeshika nafasi ya Nkosazana Dlamini Zuma baada ya wagombea wa nafasi hiyo kushindwa kupata kura za kutosha. 

Msemaji wa Zuma, Jacob Enoh Eben amesema kuwa moshi mweusi ulifumuka jana katika kikao cha kuchagua Kamishna Mkuu mpya wa AU, suala lililoashiria kwamba viongozi wa Afrika wameshindwa kuchagua kiongozi mpya wa jumuiya hiyo kubwa zaidi barani Afrika. Enoh Eben amesema kuwa uchaguzi wa Kamishna Mkuu mpya wa Umoja wa Afrika utafanyika katika mkutano wa Januari mwakani.

Ajenda kuu ya mkutano wa Kigali ilikuwa mjadala wa haki za binadamu hususan wanawake, uchaguzi wa Kamishna Mpya wa umoja huo na mgogoro wa ndani huko Sudan Kusini. 

Katika mkutano wa Kigali viongozi wa Afrika walizindua hati mpya ya kusafiria ya Afrika itakayonza kutumiwa na viongozi na maafisa wa serikali na taasisi muhimu barani humo.