Afrika kupata chanjo za mpox karibu milioni moja
(last modified Thu, 29 Aug 2024 07:42:10 GMT )
Aug 29, 2024 07:42 UTC
  • Afrika kupata chanjo za mpox karibu milioni moja

Wakala wa Afya wa Umoja wa Afrika jana ulieleza kuwa unakaribia kupata karibu dozi milioni moja za chanjo ya mpox, na kuwataka wazalishaji kuzipatia taasisi nyingine teknolojia ya kutengeneza chanjo ya mpox ili kukabiliana na ugonjwa huo.

Katika hali ambayo Afrika iko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya mpox, Shirika la Afya Duniani (WHO) mapema mwezi huu lilitangaza dharura ya kimataifa kutokana na kuenea kwa ugonjwa huo wa virusi.

Jeann Kaseya Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) ameliambia kongamano la kikanda la WHO lililofanyika katika Jamhuri ya Kongo kuwa bara la Afrika linaelekea kupata karibu dozi milioni moja za mpox.  

Nchi kadhaa zimeahidi kupeleka chanjo katika nchi za Kiafrika zilizokumbwa na milipuko, huku Uhispania pekee ikiahidi dozi 500,000.

Kaseya ameeleza kuwa dozi 215,000 za chanjo ya ugonjwa wa mpox tayari zimepatikana kutoka kiwanda cha uzalishaji dawa cha Denmark cha Bavarian Nordic hata hivyo amekihimiza kiwanda hicho kuzipatia nchi nyingine teknolojia ya uzalishaji ili ziweze kujizalishia zenyewe chanjo hiyo.

Ugonjwa wa mpox ambao awali ulijulikana kama monkeypox, ni ugonjwa wa virusi unaoambukizwa kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu ambao unaweza pia kusambaa kutoka kwa binadamu hadi kwa binadamu, na kusababisha homa, maumivu ya misuli na vidonda vya ngozi.

Maambukizo ya mpox 

Shirika la Afya Duniani limesema kuwa, jumla ya watu 5,281 wameambukizwa virusi vya mpox tangu kuanza mwaka huu wa 2024 hadi tarehe 25 mwezi huu wa Agosti.