Walioshiriki maandamano dhidi ya serikali Nigeria wafunguliwa mashtaka ya uhaini
Nigeria siku ya Jumatatu iliwafungulia mashtaka ya uhaini watu 10 walioshiriki katika maandamano ya kuipinga serikali yaliyofanyika nchi nzima mwezi uliopita.
Waandamanaji 10 walishtakiwa mbele ya Mahakama Kuu ya Shirikisho huko Abuja, mji mkuu wa nchi hiyo baada ya kukamatwa na polisi.
Mwendesha mashtaka wa serikali amesema katika hati ya mashtaka kwamba vitendo vya waandamanaji wakati wa maandamano ya Agosti 1-10 ni sawa na uhaini na uchochezi wa jeshi kupindua serikali ya kidemokrasia.
Mawakili wa waandamanaji hao waliiomba mahakama kuwapatia washtakiwa hao dhamana kabla ya kufunguliwa kesi hiyo Septemba 11.
Hakimu, hata hivyo, aliamuru kuwa waandamanaji wazuiliwe katika gereza katika mji mkuu wa taifa hilo wakisubiri kuamuliwa kwa ombi la dhamana lililopangwa kuchunguzwa Septemba 11.
Maelfu ya vijana, wanaharakati, na wanasheria walifanya maandamano ya siku 10 nchini kote kupinga gharama kubwa ya maisha, matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa usalama katika taifa hilo la Afrika Magharibi ambapo walipuuza ombi la Rais Bola Tinubu la kusitisha maandamano hayo ambayo baadaye yalibadilika na kuwa vurugu na uharibifu wa majengo ya umma. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamedai kuwa watu 21 waliuawa katika maandamano hayo.