Lugha ya Kirusi yaanza kufundishwa bure nchini Niger, pigo kwa Kifaransa
Masomo ya bure ya lugha ya Kirusi yalizinduliwa rasmi jana Jumatatu katika Jumba la lugha ya Kirusi huko Niamey, mji mkuu wa Niger na kuvutia idadi kubwa ya wanafunzi. Hii ni ishara ya kupigwa teke lugha za nchi za Magharibi hasa Kifaransa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Ikumbukwe kuwa Niger ni nchi ambayo Ufaransa ilikuwa inajifaragua inavyotaka ndani yake.
Waendeshaji wa mradi huo wamesema kuwa huo ni mpango kabambe unaolenga kufungua mitazamo mipya ya kitamaduni na kiisimu kwa wanafunzi wa Niger na kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, masomo hayo yamekusudia kuwatayarisha wanafunzi na watu wengine wanaotaka kwenda Russia, ili wawe na ufahamu wa lugha ya Kirusi wa kuwawezesha kuwa na mawasiliano mazuri na wazungumza wa lugha hiyo.
Tarehe 12 Juni mwaka huu, Jumba la lugha ya Kirusi ambayo ni taasisi isiyo ya kiserikali, lilizinduliwa huko Niamey. Mkurugenzi wake, Bello Issoufou, amesema kuwa, kufunguliwa taasisi hiyo ya kitamaduni kunaonesha kuzidi kuimarika uhusiano kati ya Niger na Russia.
Kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa Niger, Ali Mahaman Lamine Zeine alikuwa amesema kwamba nchi yake inataka kutanua ushirikiano wake wa kiuchumi na kiusalama na Russia. Waziri Mkuu huyo aliliambia shirika la habari la Sputnik mwezi Januari mwaka huu kwamba Niger inataka kuimarisha uhusiano wake na Russia katika maeneo ya biashara na kilimo.
Niamey, mji mkuu wa Niger, ulikaribisha ufunguzi wa Kituo cha Lugha ya Kirusi na Kiutamaduni siku ya Ijumaa ambapo chuo kikuu cha Russia kilisaidia kuanzishwa kwake.
Kituo hicho kipya kwa kifupi RUDN cha kuimarisha urafiki na watu Russia, kimefunguliwa huko Niger kwa msaada wa serikali ya Russia.