IOM: Tumeokoa wahamiaji haramu 979 katika pwani ya Libya wiki iliyopita
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilitangaza jana Jumatatu kuwa, wahamiaji 979 wameokolewa na kurudishwa nchini Libya katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
Sehemu moja ya taarifa ya IOM imesema: "Kuanzia tarehe 25 hadi 31 Agosti 2024, wahamiaji 979 walizuiwa kuendelea na safari za hatari na kurudishwa Libya.
"Wahamiaji hao ni pamoja na wanawake 74 na watoto 33," imesema taarifa ya IOM na kuongeza kuwa, miili saba ya wahamiaji haramu ilipatikana na wengine wanane walitoweka katika pwani ya Libya na hadi sasa hawajapatikana.
Vile vile imesema: "Jumla ya wahamiaji 15,117 wameshaokolewa mwaka huu, wakati 434 wamethibitishwa kufa maji na wengine 611 wamepotea baharini na hadi hivi sasa hawajapatikana.
Kwa mujibu wa shirika hilo la kimataifa la uhamiaji, wahamiaji 17,190 walizuiliwa kuendelea na safari na kurudishwa Libya mwaka jana 2023.
Tangu ulipoanguka utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011 na kupelekea kukosekana utulivu nchini Libya, hali hiyo inatumiwa vibaya kufanyia magendo ya binadamu hasa kutoka nchi za Afrika watu ambao wanahatarisha mno maisha yao kwa tamaa za alinacha za eti kupata maisha bora barani Ulaya.