Rais Xi wa China aahidi ajira milioni moja kwa bara Afrika
Rais wa China Xi Jinping ameahidi kuunda nafasi za kazi zaidi ya milioni moja barani Afrika huku akijaribu kuiweka Beijing kama mshirika bora wa maendeleo kwa nchi za Eneo la Kusini mwa Dunia.
Akizungumza kwenye Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika leo Alhamisi, Xi amesema Beijing itatoa dola bilioni 51 kwa nchi za Afrika katika ufadhili mpya, ikiwa ni pamoja na mikopo na "aina mbalimbali za misaada", na kuunga mkono miradi 30 ya miundombinu ili kuimarisha mawasiliano katika bara zima.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Xinhua, Xi amewaambia viongozi wa Afrika waliotembelea Beijing kuwa: "Tumejenga kwa pamoja barabara, reli, shule, hospitali, maeneo ya viwanda na maeneo maalumu ya kiuchumi. Miradi hii imebadilisha maisha na hatima ya watu wengi."
Rais Xi amesema kuwa watu wa China na Afrika wanaofanya kazi pamoja wanaweza "kufanikisha mambo mapya na makubwa zaidi" na kuongoza "kisasa" Eneo la Kusini mwa Dunia.
Tamko la Rais Xi limekuja wakati Beijing inatafuta kupanua ushawishi wake barani Afrika huku kukiwa na tofauti za kiuchumi na kidiplomasia kati ya nchi za Magharibi, hasa Marekani.
Mchakato wa Beijing wa kuimarisha zaidi uhusiano na Afrika pia unakuja wakati uchumi huo wa pili kwa ukubwa duniani ukipungua chini ya changamoto ambazo ni pamoja na tatizo la muda mrefu katika sekta ya nyumba na kupungua kwa idadi ya watu.
Katika kuelekea mkutano wa kilele wa siku tatu, viongozi wa Afrika walitangaza mikataba mingi kuhusiana na ushirikiano katika miundombinu, kilimo, madini na nishati.
Kwa mfano Rais William Ruto wa Kenya alitangaza mipango ya kushirikiana na China katika upanuzi wa reli kati ya mji mkuu Nairobi na Mombasa ili iweze kufika katika mpaka na Uganda na barabara kuu magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.