Niger yawakamata mamia ya magaidi huku operesheni za usalama zikiendelea
Mamlaka nchini Niger imewakamata takriban watu 245 wanaoshukiwa kuwa ni magaidi katika operesheni zinazoendelea za kukabiliana na ugaidi, uhalifu na uasi.
Kukamatwa kwa watu hao kulitekelezwa na Kikosi cha Idara Kuu ya Niger ya Mapambano dhidi ya Ugaidi na Uhalifu wa Kimataifa Ulioratibiwa.
Taarifa ya wakuu wa Niger siku ya Alhamisi imesema wengi wa waliozuiliwa wanashukiwa kuwa wanachama wa makundi ya kigaidi yanayojihusisha na utekaji nyara na vitendo vingine vya uhalifu, kwenye mpaka wa Niger na Nigeria, katika ngome ya magaidi ya Boko Haram.
Magaidi wengine walikamatwa karibu na mpaka wa Mali na Niger, eneo ambalo kuna magaidi wanaofungamana na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda. Miongoni mwa waliokamatwa ni raia kutoka Algeria, Chad na Somalia.
Niger, pamoja na nchi jirani za Burkina Faso na Mali, zimewafukuza wanajeshi wa Ufaransa na nchi zingine za Magharibi waliokuwa katika nchi hizo wakidai kupambana na ugaidi. Licha ya kuwepo askari hao wa Magharibi ugaidi uliongezeka katika eneo hilo.
Mapema mwaka huu, mataifa hayo matatu yaliunda Muungano wa Nchi za Sahel na kutangaza kuundwa kwa kikosi cha pamoja cha kijeshi ili kukabiliana na ongezeko la changamoto za kiusalama zinazoletwa na makundi ya kigaidi katika eneo hilo.