DRC yapokea shehena ya kwanza ya chanjo ya mpox ili kuzuia kuenea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116064-drc_yapokea_shehena_ya_kwanza_ya_chanjo_ya_mpox_ili_kuzuia_kuenea
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imepokea shehena yake ya kwanza ya chanjo ya mpox kusaidia kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo nchini humo.
(last modified 2024-09-06T03:58:10+00:00 )
Sep 06, 2024 03:58 UTC
  • DRC yapokea shehena ya kwanza ya chanjo ya mpox ili kuzuia kuenea

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imepokea shehena yake ya kwanza ya chanjo ya mpox kusaidia kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo nchini humo.

Mkurugenzi Mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) Daktari Jean Kaseya amesema katika taarifa yake ya pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwamba shehena ya kwanza ya karibu dozi 100,000 za chanjo ya JYNNEOS iliwasili Alhamisi nchini DRC na dozi za ziada 100,900 zitawasili kesho.

Kaseya amesema hadi mwisho wa wiki, dozi 200,000 zitapatikana nchini DRC -- nchi ambayo imeripoti zaidi ya kesi 4,901 zilizothibitishwa, na vifo  zaidi ya 629, tangu kuanza kwa 2024.

Aliongeza kuwa kupokea chanjo hizi ni hatua muhimu katika mapambano dhidi ya mpox haswa  kwa ajili kulinda afya ya watoto ambao wako hatarini zaidi.

Waziri wa Afya wa DRC Samuel Roger Kamba naye alisema katika taarifa yake kwamba wizara yake "ina furaha kwamba inaweza kukabiliana na Dharura ya Afya ya Umma ya Kimataifa katika kwa kuhakikisha kuwa chanjo zinawasili nchini humo kwa wakati.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yenye watu wapatao milioni 100 iko kwenye kitovu cha mlipuko wa mpox ugonjwa ambao Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa ni dharura ya afya ya umma duniani mwezi uliopita.