Mzee wa miaka 75 jela miaka 20 kwa mauaji ya kimbari Rwanda
Mzee mmoja wa miaka 75 amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela nchini Rwanda baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya kimbari.
Ripoti zinasema, Rwanda imempata na hatia mzee mwenye umri wa miaka 75 ya kushiriki katika mauaji ya kimbari ya 1994, na kumhukumu adhabu ya miaka 20 jela.
Venant Rutunga alirejeshwa kutoka Uholanzi hadi Rwanda mwaka 2021, ambako alifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ktuelekeza mauaji ya kimbari ya Rwanda.
Mwendesha mashtaka alisema mashahidi walimhusisha Rutunga kwa kuwaleta maafisa wa polisi kwenye taasisi ya utafiti wa kilimo (ISAR), ambako aliwahi kuwa mkurugenzi wa mkoa, kupelekea wafanyakazi Watutsi na wale waliotafuta hifadhi huko kuuawa.

Kitengo cha Mahakama Kuu ya Uhalifu wa Kimataifa kilimuhukumu “Venant Rutunga” miaka 20 jela kwa kuhusika kwake katika mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi,” kulingana na chombo cha habari kinachoungwa mkono na serikali, New Times.
Awali, mshtakiwa huyo alikabiliwa na mashtaka matatu: Mauaji ya kimbari, kushiriki katika mauaji ya kimbari, na kushiriki katika mauaji ya kuangamiza kama uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Hata hivyo, jopo la majaji watatu liliamua kwamba hakuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa Rutunga alishiriki binafsi katika mauaji au kutoa silaha. Waendesha mashtaka walikuwa wameomba kifungo cha maisha.
Rutunga ambaye alikana mashtaka dhidi yake, alidai kuwa aliwaita maafisa hao wa polisi ili kulinda usalama wa taasisi hiyo, uamuzi ambao amesema uliidhinishwa na bodi ya wakurugenzi ya ISAR.