Sep 08, 2024 06:53 UTC
  • Tebboune atazamiwa kushinda uchaguzi wa rais Algeria

Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea baada ya uchaguzi wa rais wa Algeria hapo jana ambapo rais aliyeko madarakani Abdelmadjid Tebboune anatarajiwa kushinda muhula wa pili.

Tebboune, mwenye umri wa miaka 78, anatazamiwa kumshinda mhafidhina mwenye msimamo wa wastani Abdelaali Hassani Cherif na mgombea wa kisoshalisti Youcef Aouchiche.

Zaidi ya Waalgeria milioni 24 walijiandikisha kupiga kura mwaka huu, na karibu theluthi moja wako chini ya umri wa miaka 40.

Tume ya uchaguzi ANIE imetangaza mapema leo Jumapili kuwa takribani asilimia 48  waliotimiza masharti walijitokeza kupiga kura.

Tume hiyo imesema idadi hiyo ni ya "muda", na kuwa itatoa idadi rasmi ya waliojitokeza baadaye Jumapili pamoja na matokeo ya uchaguzi.

Tangazo hilo limekuja saa tatu nyuma ya ratiba baada ya tume ya uchaguzi kusema Jumamosi jioni kwamba ilikuwa imeongeza upigaji kura kwa saa moja, ikitarajia wapiga kura zaidi watajitokeza.

Katika kipindi chote cha utawala wake, Tebboune ametumia mapato ya mafuta na gesi kuongeza huduma za kijamii - ikiwa ni pamoja na bima ya ukosefu wa ajira na vile vile mishahara ya umma na pensheni katika nchi hiyo kubwa zaidi barani Afrika  ambayo ina karibu watu milioni 45.