Khartoum yakataa kikosi cha Umoja wa Mataifa kutumwa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116164-khartoum_yakataa_kikosi_cha_umoja_wa_mataifa_kutumwa_sudan
Serikali ya Sudan imekataa wito wa Umoja wa Mataifa wa kutumwa "kikosi huru kisichoegemea upande wowote" kuwalinda mamilioni ya raia waliolazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na vita vinavyoendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
(last modified 2024-09-09T00:31:57+00:00 )
Sep 09, 2024 00:31 UTC
  • Jenerali Abdel Fattah al-Burhan
    Jenerali Abdel Fattah al-Burhan

Serikali ya Sudan imekataa wito wa Umoja wa Mataifa wa kutumwa "kikosi huru kisichoegemea upande wowote" kuwalinda mamilioni ya raia waliolazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na vita vinavyoendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan, ambayo iko chini ya jeshi linaloendeswa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, imesema kwenye taarifa yake kwamba "serikali ya Sudan inakataa mapendekezo yote ya kuwa na kikosi cha Umoja wa Mataifa."

Mbali na kukataa wito wa timu ya wataalamu ya kuwekwa marufuku ya silaha dhidi ya Sudan, taarifa hiyo iliongeza pia kwamba jukumu la Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa ni kusaidia mchakato wa kitaifa, badala ya kusaka njia ya kuleta mifumo ya nje kuingilia mambo ya ndani."

Hayo yanajiri katika hali ambayo, ujumbe Huru wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa kutafuta ukweli nchini Sudan, umetoa wito wa kuwekwa vikwazo vya silaha kote nchini Sudan kutokana na kukithiri vitendo vya kikatili zikiwemo hujuma za kutisha za kingono.

Majenerali hasimu ambao wameitumbukiza Sudan katika vita na machafuko

 

Sudan imekumbwa na vita kati ya jeshi, linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni mkuu wa Baraza la Mpito la Utawala, na kundi la RSF linaloongozwa na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, takriban watu 12,260 wameuawa na zaidi ya 33,000 kujeruhiwa katika vita vilivyoanza Aprili 2023,

Mgogoro wa kibinadamu unaendelea kuwa mbaya zaidi kwani karibu watu milioni 6.8 wamekimbia makazi yao kutafuta usalama nchini Sudan au nchi jirani. Jitihada za kieneo na kimataifa hadi sasa ziimeshindwa kukomesha mapigano hayo.