Somalia yafanya mkutano wa usalama na wa hali ya hewa mjini Mogadishu
Somalia jana Jumatatu ilifanya Kongamano muhimu la Usalama na Hali ya Hewa katika mji mkuu Mogadishu, ukiwa ni mkutano muhimu wa mabadiliko ya hali ya hewa na kulinda usalama wa taifa.
Mkutano huo uliofunguliwa na Naibu Waziri Mkuu Salah Jama umeandaliwa na ofisi ya Mshauri wa Usalama wa Taifa na kuwakusanya pamoja maafisa wakuu wa serikali na wawakilishi kutoka mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
Christophe Hodder, mshauri wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya hali ya hewa na mazingira nchini Somalia amesema: "Mkutano wa leo (jana Jumatatu) ni muhimu sana kwa sababu umewaleta pamoja watu wanaoupa umuhimu usalama wa hali ya hewa ili kujadiliana watu wanaohusika na masuala ya usalama wa vitengo tofauti."
Vilevile amesisitizia haja ya kuongezwa juhudi zilizoratibiwa vyema za kukabiliana na changamoto za siku zijazo za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa usalama.
Somalia imekumbwa na changamoto kali zinazohusiana na hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na ukame mbaya zaidi wa mwaka jana 2023 ambao haujawahi kutokea katika miongo kadhaa, ikifuatiwa na mafuriko makubwa.
Mbali na changamoto za hali ya hewa, Somalia inaendelea kupambana na ukosefu wa utulivu unaotokana na mashambulizi ya genge la kigaidi la al-Shabaab ambalo limekuwa likifanya mashahmbulio ya mara kwa mara na kuisababishia migogoro serikali ya Somalia ambayo inasaidiwa na askari wa Umoja wa Afrika tangu mwaka 2007 kupambana na genge hilo na kurejesha amani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.