DRC yapokea dozi 50,000 za chanjo dhidi ya Mpox
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, dozi 50,000 za chanjo dhidi ya Mpox ziliwasili Jumanne ya juzi, wiki moja baada ya shehena ya kwanza kutoka Umoja wa Ulaya kuwasili nchini humo.
Cris Kacita Osako, mratibu wa kamati ya Congo ya kukabiliana na Monkeypox amesema kuwa, watu wazima huko Equateur, Kivu Kusini na Sankuru, majimbo matatu yanayoathirika zaidi, ndio watapewa chanjo hiyo kwanza, kuanzia tarehe 2 Oktoba.
Wiki iliyopita, shehena ya kwanza ya chanjo ya mpox iliwasili katika mji mkuu wa DRC, kitovu cha mlipuko huo.
Dozi 100,000 aina ya JYNNEOS zilizotengenezwa na kampuni ya Denmark, Bavarian Nordic, zilitolewa kama msaada na Umoja wa Ulaya kupitia idara yake ya majanga ya afya (HERA). Dozi nyingine 100,000 zilitolewa mwishoni mwa Juma.
Dozi hizo 50,000 zilizotolewa na Marekani ni aina hiyo hiyo ya chanjo ya JYNNEOS.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yenye watu zaidi ya milioni 100 iko kwenye kitovu cha mlipuko wa mpox ugonjwa ambao Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa ni dharura ya afya ya umma duniani mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani - WHO, karibu visa 15,000 vya mpox vimegundulika nchini Kongo katika mwaka wa 2024, huku kukiwa na vifo 500.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, licha ya kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, lakini vifo vinavyotokana na maradhi hayo ni vichache.