Majenerali hasimu Sudan wasema wako tayari kutafuta suluhu ya vita
Pande hasimu nchini Sudan ambazo zimeitumbukiza nchi hiyo katika vita zimetangaza kuwa ziko tayari kwa ajili ya kuhitimisha vita hivyo.
Mkuu wa Baraza la Utawala wa Mpito na Kamanda wa Jeshi la Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan, pamoja na hasimu wake Muhammad Hamdan Dagaloanayeongoza Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) kwa pamoja wamesema kuwa, wako tayari kutafuta suluhu ya vita vinavyoendelea nchini humo kwa miezi 17.
Hata hivyo majenerali hao wawili wameendelea kulaumiana kwa kushindwa kumaliza mapigano na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya raia, bila yao kuweka bayana, mikakati ya kufikia mwafaka kwa njia ya amani.
Huku Mkuu wa Baraza la Utawala wa Mpito na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan, amekuwa akisisitiza kwamba hatafanya mazungumzo na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) maadamu vita vinaendelea.
Wakati huo huo, mashirika ya misaada ya kibinadamu yamekuwa yakilaani ukosefu wa usalama unaotatiza utoaji wa misaada, huku zaidi ya watu milioni 25 wakisumbuliwa na uhaba wa chakula na hatari ya njaa nchini Sudan.
Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana (2023) kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.
Hadi sasa juhudi za upatanishi wa kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo na kuzishawishi pande hasimu kuketi kwenye meza ya mazungumzo zimegonga mwamba.