Watu 70 wauawa kaskazini mashariki mwa Kongo; Umoja wa Mataifa walaani ghasia
Kwa uchache watu 70, wengi wao wakiwa raia, wameuawa katika shambulio lililofanywa na watu wenye silaha waliohusishwa na wanamgambo wa CODECO, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Shambulio hilo ni la hivi karibuni zaidi katika mfululizo wa mashambulizi yanayofanyika katika jimbo la Ituri lenye utajiri wa dhahabu, ambalo linapakana na Uganda na limekumbwa na machafuko kwa miaka mingi.
Vyanzo vimeripoti kwamba shambulio hilo, lililotokea mwishoni mwa Aprili, lilifanywa na wanamgambo wa CODECO, ambao wanadai kutetea haki za kundi la kabila la Lendu, ambao kimsingi ni wakulima, dhidi ya kundi la kabila la Hema, ambao wengi wao ni wafugaji.
Ripoti zinasema, ukusanyaji wa maiti za waathiriwa umecheleweshwa kwa siku kadhaa kutokana na ukosefu wa usalama katika eneo hilo.
Vyanzo vya usalama viliripoti vifo 70, huku Dieudonné Lussa, afisa wa asasi ya kiraia katika jimbo la Ituri (kaskazini mashariki), akisema idadi ya awali ya vifo kutokana na shambulio hilo "inazidi 70."
Vikundi kadhaa vya waasi vinafanya harakati katika eneo hilo, hasa Allied Democratic Forces (ADF), iliyoundwa na waasi wa zamani wa Uganda na Congress for the Popular Revolution (CPR), ambalo linadai linatetea maslahi ya kabila la Hema.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) umelaani "wimbi la mashambulizi yanayowalenga raia" katika majimbo ya mashariki mwa nchi hiyo.
MONUSCO imeripoti kwamba "makumi ya raia wameuawa katika siku za hivi karibuni" katika maeneo kadhaa yaliyoko katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini (mashariki), bila kutoa maelezo zaidi kuhusu mazingira ya mashambulizi hayo na idadi ya waathiriwa.