Rwanda yaanza zoezi la kutoa chanjo ya Mpox
Wizara ya Afya ya Rwanda imetangaza kuwa, imeanza zoezi la kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa ya Mpox.
Kama ilivyotangazwa na afisa mkuu kutoka kituo cha Afrika cha kudhibiti magonjwa, Rwanda imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuanza kutoa chanjo hiyo mwezi wa saba mwaka huu.
Rwanda ilithibitisha wagonjwa wawili wa kwanza wa Mpox lakini hakuna aliyeripotiwa kufariki dunia hadi hivi sasa.
Kulingana na Daktari Nicaise Ndembi kutoka Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Magonjwa, Rwanda imekuwa nchi ya kwanzakutoa chanjo dhidi ya homa ya nyani – ambapo kwa mjibu wa wizara ya afya ya Rwanda zoezi la kutoa chanjo hiyo ni kuanzia, "wafanyabiashara wa mipakani, wahudumu wa afya, wafanyakazi wa hoteli na wengine walioko katika hatari ya kuambukizwa kwa urahisi".
Chanjo ambayo Rwanda ilianza kutoa ni dozi 1,000 ilizopewa na Nigeria miongoni mwa dozi 10,000 ambazo Marekani ilitoa kwa Nigeria mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti, kulingana na maafisa wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Magonjwa.
Agosti 14 mwaka huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza hali ya dharura ya kimataifa kutokana na kusambaa kwa virusi vya mpox, hasa kuongezeka kwa visa vya maambukizi vya aina mpya ya virusi hivyo inayofahamika kama Clade 1b nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa mujibu wa WHO, kanda ya Afrika hivi sasa inashuhudia ongezeko la maambukizo ya homa hiyo, huku mataifa 14 ya bara hilo yakiathirika.
Shirika la Afya Duniani limetangaza kuwa, licha ya kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, lakini vifo vinavyotokana na maradhi hayo ni vichache.