UNHCR: Wakimbizi Afrika Magharibi, Kati wafikia milioni 14
Shirika la Kuhuduumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, idadi ya wakimbizi na watu waliolazimishwa kuyahama makaazi yao katika eneo la Afrika Magharibi na Kati imeongezeka maradufu tangu mwaka 2019.
Kamishna Mkuu wa UNHCR kanda ya Afrika Magharibi na Kati, Abdouraouf Gnon-Konde, amewaambia waandishi habari mjini Abidjan kuwa idadi hiyo imepanda kutoka wakimbizi milioni 6.5 mwaka 2019 hadi milioni 13.7 mwaka huu.
Gnon-Konde amesema kufikia mwishoni mwa mwaka huu, idadi hiyo huenda ikaongezeka hadi kufikia kati ya watu milioni 14 na 15.
Hata hivyo, Kamishna Mkuu wa UNHCR idadi hiyo haijumuishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako UNHCR inakadiria kuwa, karibu watu milioni saba wamelazimika kuyahama makaazi yao.
Kutokana na kwamba watu wengi waliokimbia makaazi yao wanashindwa kurejea nyumbani kwa miongo kadhaa, Shirika la Kuuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limezitaka nchi zinazowahifadhi wakimbizi hao kuwajumuisha katika mipango yao ya maendeleo.
Wakimbizi ni sehemu muhimu na kubwa katika jamii ya mwanadamu duniani leo. Takwimu za karibuni kabisa zinaonesha kuwa, sasa hivi kuna zaidi ya wakimbizi milioni 82 katika kona mbalimbali za dunia. Idadi hiyo inaunda zaidi ya asilimia moja ya watu wote ulimwenguni na ni sawa na idadi ya watu wa nchi moja kubwa duniani.
Kiujumla kuna aina tatu za jamii ya wakimbizi duniani. Wakimbizi wa ndani ya nchi ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na sababu mbalimbali. Idadi ya wakimbizi wa ndani kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa ni watu milioni 48.